Tangazo

TANGAZO No 44 /2015 LA CHAMA CNDD-FDD LA TAREHE 14 DESEMBA 2015

 » Mbelgiji Louis Michel anashauri watu wake kubadilishana madaraka ya utawala wa nchi kwa kuzingatia ukabila kwani anajua kuwa ndiyo kifo cha demokrasi ».

  1. Tarehe 23 Novemba, 2015, Mwenyekiti wa shirika binafsi la kupambana na rushwa hapa Burundi (OLUCOME) Ndugu RUFYIRI Gabriel, alimuandikia Rais wa Uganda Mheshimiwa Yoweli Kaguta Museveni barua N° 049/Olucome/2015. Kichwa cha barua hiyo ni : Mwaliko wa mazungumzo ya haraka ili kuilinda Burundi na Ukanda wa nchi za Maziwa Makuu. Barua hiyo ina uongo mwingi na maneno ya kukichafua chama CNDD-FDD na serikali yake. Bwana RUFYIRI alisaini na kutuma barua iliotungwa na wengine. Aliyeagiza barua hiyo alijifanya muhusika wakati siye. Uongo wa pili ni kwamba Gabriel RUFYIRI anataka kuchukulia OLUCOME kama mpatanishi akidhani kuwa asasi yake iko juu ya nyingine. Ikumbukwe kuwa tangu mwaka 2005 shirika lake halikuchoka kuitakia nchi na wananchi wake mabaya kupitia matangazo. Hayo yote yalikuwa na madhumuni ya kuchochea maovu na kutenganisha wananchi. Wakati wote alikuwa akijifanya msamalia mwema wakati ni umbwa mwitu kisiasa. Anajifanya muungwana wakati moyo umejaa unafiki, bila shaka anashauriwa na msimamizi wake. Kwa vyovyote haitamfikisha popote, wala haimdanganyi mtu. Uongo mwingine ni kudai kuwa anaipenda nchi wakati moyoni mwake kuna hila ya kuwapinga na kutowapenda Warundi kwa ujumla hususan wanachama wa CNDD-FDD na serikali yake. Ikimbukwe kwamba alikuwa miongoni mwa waliyoiombea nchi vikwazo vya misaada na kuitenga nchi yake mwenyewe bila kusahau kuichafua Serikali kupitia matangazo yenye kashfa na uzushi mwingi wa aibu ;
  1. Katika barua hiyo iliyopelekwa kwa Rais wa Uganda ukurasa wa 8, mstari wa 24, inaweka wazi na kudai kuwepo kwa mgawanyo wa madaraka kwa kuzingatia ukabila. Wazo lililopigwa vita hata katika mazungumzo ya Arusha. Inaonekana kuwa msimamo huo haujafutika vichwani miongoni mwa waliohudhuria mazungumzo ya Arusha. Kwa kifupi, kubadilishana madaraka ya uongozi wa nchi wanakotaka ni kama kupokezana madaraka kwa misingi ya ukabila. Na tangu ushindi wa chama CNDD-FDD wa 2005, kauli kama hizo ziliendelea kutamkwa na baadhi ya wanasiasa wa upinzani na hasa waliowahi kuwa madarakani wakati wa tawala za kijeshi. Tawala zilizosababisha vifo vingi tangu nchi ilipopata uhuru ;
  1. Kubadilishana madaraka kwa msingi wa kikabila kuna maana ya kukataa au kudharau makubaliano ya Arusha, kwani kugawana madaraka kwa misingi ya idadi ya makabila itaweka mbele maslahi ya ukabila. Ina maana kabila moja litawale miaka 5 kuanzia ngazi ya juu hadi ngazi ya chini na kabila jingine hivyo hivyo kipindi kingine kinachofuata cha miaka 5. Kwa utaratibu huo, ni lini Watwa watatawala ? Na vipi makabila ya raia wengine wanaoweza kuzaliwa!. Kitu cha aibu na kusikitisha ni kwamba wenye mawazo ya kupokezana madaraka ya uongozi ndiyo walioandaa njama za kumrudisha madarakani Piere BUYOYA na kundi lake kwa malengo ya kutokomeza kabila wasilotaka. Chama CNDD-FDD kinakemea vikali tabia hiyo ya kutaka kurudisha utawala wa zamani wa ukoloni wa Ubelgiji wa tangu 1922 hadi 1962. Wakati huo sehemu moja ya wananchi ilikuwa chini ya nyingine, kana kwamba jamii moja ya warundi ni zaidi ya nyingine na kwamba ni uzao wa utawala kwa picha na msimamo wa ukoloni wa Ubelgiji. Fikra hizo zinazotumiwa na Louis Michel zina lengo la kurudisha utawala mikononi mwa wanaojiita wataule wa kutawala na kukandamiza kabila linalodhaniwa kuwa ni duni. Wazo hilo la wakoloni la kutaka kurudisha nchi hii katika utumwa ni la kupiga vita kwa nguvu zote kwani lina malengo ya kuteka na kupokonya uhuru na kujitawala kwa Warundi pamoja na uhuru wa wananchi wa kujichagulia viongozi wao wenyewe katika amani. Tofauti na hayo ni kurudisha nyuma hatua iliyofikiwa ;
  1. Mawazo hayo yafaa yafuatiliwe kwa karibu kwani wanaozungumzia ukabila wana agenda ya kuangamiza wengine kwa kuanzia wasomi wa chama CNDD-FDD kana kwamba wanachama wote ni wa kundi moja la wananchi wasio na haki ya kuongoza. Chama CNDD-FDD kinasikitishwa na ukimya wa Ubelgiji kwa hali hiyo ya kutisha na jinsi Wabelgiji wanavyoyaamuru Serikali ya CNDD-FDD kuzungumza na hao wafanyao ugaidi na waliojaribu kuiangusha serikali iliyochaguliwa na wananchi. Ingekuwaje kama mauaji ya namna hii yangefanyika nchini mwao ? Mfano yaliyofanyika Ufaransa yanaweza kuwapa somo, hakuna maelezo zaidi. Serikali ya Ubelgiji ni sawa na serikali ya Burundi kwa misingi ya haki na uhuru wa Taifa, kwa nini wanajishughulisha na kutaka kuondoa uongozi uliochaguliwa kidemokrasi 2015 ? Yote hayo ni kusaidia viongozi wa tawala za waliofanya mauaji ya 1965, 1988 na mauaji ya kimbali ya kati ya mwaka 1972 – 1973 na mengine dhidi ya viongozi wa Burundi wa serikali zilizofuatana hadi kabla ya tarehe 16 Novemba 2003 uliposainiwa Mkataba wa kukomesha vita ;
  1. Unasikitisha uvamizi wa tarehe 11 Desemba 2015 dhidi ya kambi tatu za kijeshi jijini Bujumbura. Uvamizi huo ulifanywa na wahalifu kwa kutumia silaha nyingi, wakiwemo vijana wengi waliodanganywa kama ilivyotangazwa na msemaji wa kijeshi. Kumiliki silaha na kujua matumizi yake ni vitu viwili tofauti . Chama CNDD-FDD hakitambui hata kidogo jinsi nchi ya Ubelgiji ikiongozwa kimakosa na Louis Michel na washirika wake kwa kuwawezesha kwa hali na mali wahalifu ikiwa ni pamoja na kuwapa silaha. Hao wanakuwa wepesi wa kutoa huduma na kuwatibu majeruhi. Hao wanaowapatia silaha, pesa na matibabu ndiyo wanaopaswa kuulizwa yahusuyo ugaidi wenye fikra za kikoloni zilizoletwa na Wabelgiji wakati wa ukoloni. Chama CNDD-FDD kinajua bayana kuwa Louis Michel na washirika wake wanapigania masilahi yao ya kikoloni kupitia migongo ya baadhi ya warundi, huku wakidanganya mataifa ili waungwe mkono katika uovu huo. Ndiyo sababu ni wazushi wa uongo dhidi ya Nchi yetu ya Burundi. Wanasiasa hao wanaoagiza makundi ya vijana kupambana na askari wenye nguvu, huku wakijua kuwa wanakwenda kufa ni usaliti, uhaini na kutaka kuuwa wananchi kwa makusudi. Hili ni tatizo jingine kati ya Burundi na Ubelgiji na wafanyao hayo watapaswa kujibu hoja katika yale mazungumzo ya Warundi na katika ile Kamati ya Ukweli na Maridhiano – CVR. Yapo mashirika ya Kimataifa kama UNHCR yanayosaidia kusafirisha silaha(mfano ni mtumishi wa UNHCR aliyekamatwa na silaha kutoka nchi ya Rwanda kwa kutumia gari la shirika hilo). Mashirika hayo nao ni maajenti wa wakoloni tuliowataja. Katika hayo inaongezeka listi ya waliokwisha uawawa tangu tarehe 26/04/2015 hadi sasa na kwa yote yenye sura hiyo yanayoweza kutokea. Ili kujiepusha na hayo, hao wawezeshao uhalifu huo hususan nchi ya Ubelgiji huomba Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya kukutana haraka kuichukulia vikwazo nchi ya Burundi wakati ndiyo inayoshambuliwa, badala ya kulaani na kukemea magaidi hao ;
  1. Kitu kingine cha kusikitisha ni madawa ya kulevya wanayopewa vijana, huku wakidanganywa kwenda kupambana na jeshi la Taifa na hatimaye kupoteza maisha. Wanaowatuma wao huchekelea tu kwani wako salama. Kwa unafiki wanapiga kelele kwa mashirika ya UN, AU eti waiadhibu Burundi wakati wao wenyewe ni mzigo na vyanzo vya matatizo yanayoendelea. Inasikitisha pia kusikia chombo cha habari Parga na Balais citoyen vya Burkina Faso na baadhi ya wananchi wa nchi hiyo wakichokoza nchi ya Burundi kwa sababu ya fitina na chuki ya kuona wabantu wakiongoza nchi. Wanatamani kuona utawala wa wabantu ukiangushwa kwani wanataka kuona Petero Buyoya akirejea madarakani na kundi lake. Ilishadhihirika kuwa waliotaka kuipindua serikali ya Burundi wana uhusiano na mawasiliano na baadhi ya wa Burkina Faso, wanaotaka mapinduzi Burundi ili uwepo uongozi wa kabila jingine kiujanja kupitia serikali ya mpito ya kugawana madaraka, kinyume na demokrasi. Njia hiyo haitawafikisha popote kwani si kabila la Thomas Sankara pekee litakalotawala Afrika. Hivyo wasidanganye mtu kuwa ni wapenzi wa demokrasi, wakati wanapigania masilahi yao binafsi. Haieleweki pia wakati serikali ya Burundi ikionana na Jumuiya ya Ulaya kuhusu kipengele cha 96 cha Mkataba wa Cotonou, viongozi wa Ubelgiji nao wakiandaa hujuma na vita ya kutaka kuiondoa madarakani serikali hiyo wakati huo huo. Ni dhahili kuwa mazungumzo hayo yalikuwa ya kuihadaa serikali ya Burundi. Hii inathibitishwa na kuona baadhi ya viongozi wa Ubelgiji badala ya kulaani wahalifu, wanakishutumu chama CNDD-FDD na serikali yake kwa kazi nzuri ya kumtatiza na kumpiga adui ambaye azma yake ni kuua. Wao wangefurahi kusikia kuwa nchi imetekwa na magaidi hao huku wananchi wakiuawa kikatili kama ilivyotokea katika historia, ambapo daima walikaa kimya kwani wanakuwa wamefikia masilahi yao. Maelezo haya ni ya uhakika kwani hata Pacifique Ninahazwe na Petro Karaveri Mbonimpa waliyo kwapani mwa Louis Michel-Ubelgiji walikuwa wanatangaza kuwa mauaji ya kimbali yameanza nchini Burundi. Naye Adama Dieng mkuu wa jukumu la kuzuia mauaji ya kimbali katika Umoja wa Mataifa (UN) aliongezea sauti akikubalisha watu kuwa mauaji ya kimbali yanakwenda kutokea kana kwamba hatujui kuwa lengo lao ni moja. Ni wakati sasa chuki hiyo yenye mizizi ya moyo wa fitina ya kikoloni ya Louis Michel na washirika wake kusimama;
  1. Ingawa kuna hali isiyoridhisha katika ushirikiano wa Burundi na nchi iliyotutawala, Chama CNDD-FDD kinathibitisha kwamba si Wabelgiji wote wenye mawazo hayo, lakini kutokemea wazo la ukoloni la Louis Michel na washirika wake na nia yao mbaya ya uonevu dhidi ya chama CNDD-FDD na Serikali yake, haifariji wala kutia moyo. Wabelgiji wasiounga mkono fikra kama hizo wanapaswa kuzikemea kwa madhumuni ya kuunga mkono warundi wapenzi wa demokrasi katika vita yao ya kuutokomeza ukoloni. Tuamini usemi wa watalaamu wa lugha ya Kifaransa wanavyosema kuwa: « qui ne dit mot consent » ikiwa na maana kwamba : ‘Hata asiyesema neno anakubaliana / kuafikiana’ ;
  1. Chama CNDD-FDD kinakumbusha kwamba jaribio la kubadilishana madaraka kikabila lilitokea mwaka 1993 katika uchaguzi wa kidemokrasi, baada ya miaka mingi ya utawala wa mabavu wa kijeshi. Lakini majibu ya Rais aliyeshindwa hayakuwa mazuri pale alipotamka kuwa uchaguzi ulikuwa sensa ya kikabila. Nao washirika wa Rais huyo aliyeshindwa walieleza kuwa si uchaguzi wa demokrasi uwezao kuwapokonya utawala wa nguvu za kijeshi kupitia mapinduzi ya serikali. Kwa kuwa Louis Michel aliwaunga mkono vibaraka wake hao, alikaa kimya. Mhanga wa demokrasi akauawa kikatiri akiwa na wafuasi wake. Wakati huo Ubelgiji ilikaa kimya, haikusema lolote ! Chama CNDD-FDD kinahusisha hayo na yaliyotokea kipindi cha mauaji ya kimbali ya mwaka 1972 – 73 ambapo Ubelgiji wakati huo pia hawakusema kitu. Kitu cha ajabu ni kuona uongozi uliochaguliwa na wananchi 2015 unapotiwa hofu za kigaidi, Ubelgiji haraka sana inasimama na kudai kuwa « Msiwaguse watoto wangu, acheni waipindue serikali ». Hao nao wanaposhindwa kufikia azma yao, Ubelgiji inawaita na kuwapa hifadhi nchini mwao. Apendaye kujua na afahamu ! ;
  1. Chama CNDD-FDD kinatambua vizuri kwamba Umoja wa Ulaya wakati huu unaombwa na Jumuiya mbalimbali kutoa maelezo kuhusu suala la Burundi. Chama CNDD-FDD hakina shaka kuwa Umoja huo wa Ulaya ulipata nakala ya barua ile iliotajwa ya OLUCOME kama ilivyoshuhudiwa na warundi na jamii ya kimataifa. Barua iliyokuwa na lengo la kurudisha nyuma nchi ya Burundi katika azma yake ya kutafuta suluhu la kudumu kwa matatizo yaliyopo. Chama CNDD-FDD kinashukuru Umoja wa nchi za Ulaya kwa kutotilia maanani barua hiyo yenye dhamira mbaya, ni katika tangazo la kuhitimisha mazungumzo yake na Burundi kuhusiana na kipengele cha 96 cha makubaliano ya Cotonou. Mazungumzo hayo yalifanyika tarehe 8 Desemba, 2015. Chama pia kinashukuru Umoja wa Ulaya kwa kuheshimu na kuzingatia maamuzi ya kipengele 2248 ya Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Kimataifa katika kikao cha tarehe 12 Novemba, 2015. Ingawa baadhi ya mataifa ya Ulaya hayaridhishwi na jinsi mazungumzo hayo yalivyokwenda. Chama CNDD-FDD kinatamka wazi mbele ya Warundi na Mataifa kukubaliana na maamuzi yaliyofikiwa na njia mwafaka za ufumbuzi wa matatizo ya Burundi kwani chama kiliendelea na mwenendo mzuri katika yote yaliyowasilishwa. Kuwa Mungu Muweza wa yote alipewa nafasi ya kwanza katika kazi zote za chama, haiwezi kuwa tofauti na utashi huo ;
  • Chama CNDD-FDD kinahitimisha tangazo hili kwa kujizatiti na kuendeleza mapambano dhidi ya ubaguzi wa kikabila wa aina yoyote na daima dhamira yake ni kuwaweka Warundi katika kundi moja kwa mambo yote na popote pale na kufikia maridhiano. Chama CNDD-FDD kinakumbusha kuwa kinaafiki mazungumzo kama nyenzo ya maana ya kuleta amani, hata tangu chama kilipokuwa vuguvugu la kuteteta demokrasi. Hivyo chama hakiwezi kubadilisha leo njia ya mazungumzo, kwani tangiapo mazungumzo yamekuwa njia muhimu katika kuleta ufumbuzi wa matatizo ya Burundi. Hivyo chama CNDD-FDD kinaomba Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla na Mashirika ya kikanda bila kusahau nchi marafiki kutambua na kuiunga mkono nchi ya Burundi katika jitihada zake za kuweka mambo sawa. Kwani uhusiano na ushirikiano ni muhimu kama wasemavyo wahenga kuwa « Umoja ni nguvu ».             

 

Tangazo limetolewa Bujumbura, tarehe 14 Desemba, 2015

Mbunge Pascal Nyabenda

Mwenyekiti wa Chama CNDD-FDD

15 décembre 2015

About Author

Willy


Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *