Actualité, Tangazo

TANGAZO No 05 /2016 LA CHAMA CNDD-FDD LA TAREHE 10Machi, 2016.

Kwa nini baadhi ya wanasiasa wameanza kukataa kazi za Kamati ya Ukweli na Maridhiano (CVR) ?

1. Vurugu za maandamano zilizoanza tarehe 26 Aprili, 2015 zilikuwa na agenda ya siri ya kutekeleza mpango wa kuiangusha serikali iliyochaguliwa na wananchi tangu mwaka 2005. Ni hivyo, kwani ushindi wa CNDD-FDD ulikasirisha baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa wamefanya nchi kama shamba lao na kugawana madaraka kama wapendavyo. Hao tunawakuta katika G 7 na G 10 pamoja na watu wa nje wanaowaunga mkono ambao walihusika katika maovu yaliyogharimu maisha ya wananchi, ambapo Petro Buyoya anachukua nafasi ya kwanza. Jaribio la mapinduzi ya serikali la tarehe 13 Mei, 2015 lilikuwa na lengo kwa maadui la kuzika mpango wa demokrasi ili nchi itawaliwe kwa nguvu kama wapendavyo. Katika serikali iliyokuwa imekusudiwa, Petro Buyoya angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukweli na Maridhiano ( CVR), hii ina maana kuwa kamwe CVR haitakiwi na hao wanafiki pia waongo wasiopenda maovu waliyotenda yajulikane ;

2. Chama CNDD-FDD kimekuwa kikielezea awamu tofauti zilizoisibu historia ya nchi tangu harakati za uhuru ambapo lilijitokeza kundi dogo lililopinga na kutatiza uhuru usipatikane mapema kwa ushirikiano na wazungu, hadi kufikia hatua ya kuuawa Mhanga wa uhuru Mfalme Louis Rwagasore mwaka 1961. Wakati ule ilionekana kuwa Ubelgiji ni chanzo cha msiba huo wa Taifa. Nchi ya Ubelgiji isiwe kimya kuhusu matukio ya Burundi pia mazungumzo ya warundi hayatamweka kando Louis Michel ili ajibu hoja zitokanazo na maovu walioitendea nchi. Kama serikali ya Ubelgiji haiwezi kueleza kwa maovu yaliyotendwa na Louis Michel na washirika wake na bado wanaendelea kuitendea nchi ya Burundi, mbele ya warundi itamaanisha kuwa serikali hiyo haina uongozi na kwamba familia ya Louis Michel ina ushawishi mkubwa na kuzuia serikali isiseme kitu. Hao nao pia hawataki kusikia CVR ;

3. Nchi ya Burundi ilipitia vipindi vingi vigumu : Kuuawa kwa Waziri Mkuu wa kwanza Petro Ngendandumwe na kufuatiwa na warundi wengi wapenda demokrasi waliouawa kinyama bila hatia, wakiwemo wabunge, wasomi, wafanya biashara hao wote walimsindikiza Pierre Ngendandumwe na kuzikwa katika mashimo ya pamoja. Kwa hiyo maafisa wa kijeshi wa wakati ule na raia walioshirikiana nao wanajua vizuri walikozikwa watu hao. Hivyo viongozi wa kijeshi na washirika wao hawataki kusikia neno CVR. Pia wapo baadhi ya waumini wa Katoliki waliopotoka na kutenda kinyume cha maadili ya dini yao ambao walishirikiana na askari katika mauaji hayo. Ikumbukwe pia kuwa baadhi ya wakimbizi wa kinyarwanda nao walisaidia katika maovu hayo ikiwa ni pamoja na kushauri ndugu zao kuwahi wengine kabla, ili isiwe kama ilivyotokea kwao nchini Rwanda. Mfano hai ni kwamba nyumba nyingi za Kata ya Asiatique zilikuwa za watu wanaosakwa, mara walipouawa nyumba hizo zilikabidhiwa kwa wakimbizi wa Kinyarwanda kama shukrani kwa kushirikiana na wauaji. Hatimaye wanyarwanda waliuza nyumba hizo kwa Warabu, Wagiriki na Wahindi kwani walijua kuwa zingewaletea matatizo. Wanyarwanda walioishi Burundi wakati ule na miaka iliyofuatia, popote walipo nao pia hawataki kusikia CVR kwani tuhuma dhidi yao zitawafikisha mbele ya sheria ;

4. Kipindi kingine cha kutisha katika historia ya Burundi ni cha 1972-73 ambapo mauaji ya halaiki yalifanywa dhidi ya kabila la walio wengi kwa muda wa miezi mitatu na kugharimu uhai wa watu zaidi ya laki tatu (300.000) na mamia elfu kuikimbia nchi. Utashi wa utawala wa wakati ule ulikuwa ni kuteketeza jamii ya wapenzi wa uongozi wa demokrasi. Kama wauaji walivyokuwa wakisema kuwa demokrasi ingetajwa tena baada ya miaka mia moja. Inasikitisha kuona kuwa fikra za mauaji ya kimbali tunayosikia kipindi hiki cha 2014-2016 zina uhusiano na mawazo ya wale wahalifu waliotaka kuiangusha serikali iliyochaguliwa na wananchi kwa ushirikiano na baadhi ya wanasiasa​ mfano Louis Michel. Ni mawazo ya kisiasa yaliyokuwa yametekelezwa na utawala wa Kikoloni wa Ubelgiji ambapo hadi 1945 hakuna hata mmoja kutoka kabila la walio wengi aliyekuwa katika Taasisi na Mamlaka za Utawala wa nchi. Ubaguzi wa wakati ule nusura utekelezwe na maadui hao wa demokrasi. Hao sasa wanaona CVR kama adui mkuu kwani maovu ya wahalifu hao yatawekwa wazi hivyo mkono wa sheria uchukue nafasi yake. Kwa mantiki hiyo, hao wanachukia chama CNDD-FDD na serikali yake kwani wanajua wapende wasipende ukweli utabainika. Ndiyo maana wanatamani serikali isiyoweza kuwagusa na kuhoji maovu waliyoitendea nchi na wananchi wake. Ajabu ni kwamba kabla ya kuwepo CVR, walikuwa wanahimiza serikali iweke Kamati hiyo. Baada ya kuwekwa CVR wanadai ingesubiri na kwamba haitafikia chochote. Inasikitisha kuona G 7 na G 10 wakijiaibisha kwa kusema kuwa hawataki CVR wakati imo katika Makubaliano ya Arusha. Hao wote hawataki uwepo wa CVR ingawa baadhi yao husema kuwa wanaongoza roho za watu. Watajwa hao hueneza habari kuwa Burundi kunafanyika mauaji ya halaiki huku wakisahau kuwa kauli hiyo ni kujitakasa kinafiki uovu huo unaobubujika mioyoni mwao na kutaka kuwapakazia wengine ; wafuatao Louis Michel, Petro Buyoya, Bernard Maingain na wengineo ndicho wanachozidi wengine. Ni dhahiri « Mtu hutoa alichonacho » ;

5. Chama CNDD-FDD budi kiwajulishe wananchi na mataifa kuwa nyumba na mashamba milki ya kabila ya walio wengi walioangamizwa 1972-73, Kata za Rohero, Kiriri na sehemu nyingine vilitaifishwa na utawala wa kijeshi wa Michel Micombero wa tarehe 6 Mei, 1972 ambapo ilitolewa hukumu kwa wote waliouawa tangu tarehe 29 Aprili, 1972 na kuamrisha kutaifisha jumla mali zao. Wakati ule Jean Baptiste Bagaza ambaye sasa ni seneta alikuwa jaji katika kesi hizo za mauaji ya halaiki. Watu wote hao waliouawa walizikwa katika mashimo ya pamoja. Watawala wa kipindi kile wawe askari au wengine wakiwemo wageni walioshirikiana wanajua walipowazika watu hao. WapingaCVR wanafanya kila linalowezekana ili Kamati hiyo isifanye kazi zake na isije ikapata vielelezo na tuhuma vya kuwashtaki mahakamani ;

6. Kipindi kingine kisichosahaulika ni mauaji ya wananchi wa Tarafa za Ntega na Marangara ya mwaka 1988. Baada ya hapo vyombo vya habari vilienea nchi nzima kuuliza walionusurika 1972-73 waliomaliza Shule za Msingi. Petro Buyoya alikuwa ameandaa mauaji ya kimbali. Isingekuwa tahadhari kwa wananchi na wapenzi wa nchi waishio nje hali ingekuwa kama ilivyotokea kipindi cha 1972-73. Kwa mara nyingine tena, Petro Buyoya na askari aliowatumia wanajua mashimo walimozikwa wananchi wasio na hatia. Hebu angalia mwaka 2015 Buyoya alivyosingizia mauaji chama CNDD-FDD na serikali yake wakati mauaji ya halaiki yako damuni mwake ; hii inathibitishwa na mauaji ya Ntega na Marangara na ya vipindi vingine. Sasa atakubalije Kamati ya CVR wakati anajua kuwa atapaswa kujibu hoja kwa aliyoyafanya ? ;

7. Maafa ya 1993 yaliyogharimu uhai wa Rais wa nchi Ndadaye Merchior na baadhi ya wasaidizi wake pamoja na wananchi wengi, bado yanakumbukwa na wapenzi wa demokrasi. Wakati wa kampeni za uchaguzi mgombea kwa tiketi ya UPRONA Petro Buyoya alisema hivi : « kama wataka kujifungua na kuishi, mpigie kura Buyoya ». Kwa wasiomchagua alitekeleza azma yake kwa kutumia askari waliomtii na silaha zao kuwaangamiza wafuasi wa FRODEBU kwa kuanzia kwa Mheshimiwa NDADAYE Melchior na wasaidizi wake. Mamia elfu wakauawa kinyama na wengine wengi wakakimbia nchi na zaidi ya 570.000 wakakusanywa kwenye makambi yanayofanana na yale ya « manazi  » kwani waliangamiziwa mahali hapo. Mwaka 2015 Petro Buyoya kwa ushirikiano na Louis Michel, Marguerite Barankitse alipiga kelele kuwa Burundi inaingia katika mauaji ya kimbali wakati hayo yako damuni mwake. Ni lini Buyoya atatamani kazi za CVR ? ;

8. Chama CNDD-FDD kinasikitishwa na mpango wa walifanya jaribio la mapinduzi la tarehe 13 Mei, 2015 wa kuwateketeza wanachama (Abagumyabanga), wapenzi na wote wanaokiunga mkono chama kama ilivyotokea tangu uhuru wa nchi. Chama kinasikitishwa na visingizio dhidi yake na kuchafuliwa kwa uongozi kupitia baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya asasi za Kimataifa kwa kuzingatia mawazo yafuatayo :

i. Kuchafua mamlaka za uongozi ili uchukiwe na wananchi pamoja na mataifa ya nje ;
ii. Kukaidi uongozi kupitia ghasia na kutotii kufuata sheria ;
iii. Kufanya maandamano na fujo vinavyoambatana na mauaji ambavyo tunaita vurugu;
iv. Kujaribu kuteka kwa nguvu sehemu nyeti za Taifa kama vile radio, kambi za kijeshi, kiwanja cha ndege na vinginevyo ;
v. Kujaribu mapinduzi ya serikali iliyochaguliwa na wananchi ;
vi. Kuua kwa halaiki wapenzi wa demokrasi wanaounga mkono uongozi ;
vii. Kuomba vikosi vya Kimataifa kuja nchini kusambaratisha uongozi kwa msaada wa baadhi ya mataifa ya nje, wao waliposhindwa ;
viii. Hayo yote yanafanyika kwa uungwanji mkono wa baadhi ya mataifa ili asiwepo yeyote wa kutetea uongozi uliopo ukiingiliwa;

9. Chama CNDD-FDD kinahitimisha kwa kujulisha kuwa yaliyotajwa hapo juu ndiyo yaliyozingatiwa na walioshiriki maandamano haramu ya tarehe 26 Aprili, 2015 na ndio hao waliofanya jaribio la mapinduzi ya tarehe 13 Mei, 2015, hayo hayakutokea kwani Mungu anaipenda Burundi na watu wake. Ingawa ni hivyo chama kinaomba wenye tuhuma na wanaojishuku wafike CVR ili waseme ukweli wao badala ya kupiga vita Kamati hiyo ya Kitaifa wakiwa nje ya nchi, kwani wasemayo yanaonyesha kuwa hawazitaki Kamati hizo. Hapa ndipo wananchi wanagundua kuwa mwenendo huo ni wa wale wanaojituhumu.
Imetolewa Bujumbura, tarehe 10Machi, 2016
Na Mwenyekiti wa chama CNDD-FDD

Mheshimiwa Pascal Nyabenda

10 mars 2016

About Author

Evelyne


Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *