Actualité, Tangazo

TANGAZO No 04 /2016 LA CHAMA CNDD-FDD LA TAREHE 02 Machi, 2016

Siku ya ujio wa wataalamu wa uchunguzi wa Haki za Binadamu Ulimwenguni nchini Burundi, tarehe 29 Februari, 2016 limeonyeshwa shimo Mutakura na mmoja wa wahalifu walimozikwa watu wengi.

1. Chama CNDD-FDD kilisikitishwa kuona shimo lenye mita 12 mlimozikwa watu zaidi ya 30, waliouawa na waliofanya maandamano haramu katika kitongoji cha Mutakura Kata ya Cibitoke, Tarafa ya Ntahangwa katika Jiji la Bujumbura. Miongoni mwa wahalifu hao walisema kuwa kuna mashimo kama hayo sehemu nyingi katika Jiji la Bujumbura. Inasikitisha kuona kwamba watu wanasahau kuwa uhai ni haki ya mtu. Nani mwenye uwezo wa kuondoa uhai wa mtu ? Kipi walichokosea ? Chama CNDD-FDD kinatoa pole kwa ndugu na familia waliofiwa na wapendwa wao na kuzikwa katika shimo hilo ;
2. Wakati wa vurugu zilizoanza 26 Aprili 2015, mengi yalisemwa kupitia Vyombo vya Habari vya Kimataifa kwa kuchafua uongozi kuwa unawasakama watu. Imedhihirika kuwa watu wengi waliuawa katika Kata za walioandamana ; hayo yameelezwa na mmoja wa wauaji aliyeonyesha mahali walipozikwa. Mauaji hayo yanayosingiziwa utawala yalikuwa na agenda gani ? Ni bayana kuwa Serikali ilisingiziwa kwa mauaji hayo kwa lengo la kusambaratisha chama CNDD-FDD na serikali yake ;
3. Wapo wanahabari wa baadhi ya Vyombo vya Habari vya Kimataiafa wanaojifanya kujua na kwamba wana vifaa, maarifa na uwezo wa kutosha waliodai kuwa kuna mauaji ya kimbali yanayofanyika, na kuwa kuna mashimo walimozikwa watu waliouawa na vyombo vya usalama. Pia wapo waliothibitisha kuwa kuna picha za setilaiti zilizoonyesha mashimo mapya walimozikwa watu. Baadhi ya sehemu hizo si hapo Mutakura ? Je hao wanahabari ambao mara nyingi walikuwa katika Kata hizo za Mutakura, Jabe, Ngagara, Nyakabiga, Musaga na Cibitoke hawajui mashimo yote walimozikwa wananchi wasio na hatia ? Wataalamu hao wa UN wa haki za binadamu wanapaswa kuwajulisha Warundi, Mataifa na wanahabari wa Kimataifa wote waliofanya kazi katika mitaa hiyo ya waandamaji haramu ya tangu Mei 2015 kwa yatokanayo na uovu huo, kwani walishuhudia mauaji hayo na mazishi huku waandishi nao wakipiga picha ;
4. Chama CNDD-FDD kiliendelea kukanusha uzushi huo, sasa imedhihirika kwamba wanahabari hao walikuwa wanachafua wajibu wa mamlaka za usalama katika Mataifa ya nje. Kwa nini waandishi hao wa Kimataifa waliozoea kufika katika Kata hizo hawakuandika au kusema habari hizo ambazo ni kama walizijua ? Hivi sasa shimo la Mutakura ni kisingizio kutoka kwa maadui wa Chama CNDD-FDD na serikali yake. Uzushi na uongo wote vinakwenda kuwa wazi na wahusika wake awali walikuwa wakidai kuwa wanatetea Katiba na Mwafaka wa Arusha, watajulikana na kufikishwa mbele ya sheria. Chama CNDD-FDD kinaomba Mataifa watambue kuwa walidanganywa, hivyo waitakase nchi ya Burundi na vyombo vya usalama kwani mamlaka hizo zilisingiziwa ;
5. Chama CNDD-FDD daima kilisema kuwa nchini Burundi kuna mashimo mengi walimozikwa watu wengi tangu zamani, lakini mataifa hayakuthubutu kujaribu kusaidia kutafuta yalipo mashimo hayo. Chama CNDD-FDD kinaomba kwa msisitizo msaada wa kimataifa ili ukweli ubainike. Chama kinaomba pia yeyote anayejua yalipo mashimo walimozikwa watu wengi hususan katika Kata za vinara wa maandamano haramu kama vile Mutakura, Cibitoke, Ngagara, Musaga, Nyakabiga na Jabe. Hatuwezi kusahau pia wote waliouawa kote nchini baada ya kifo cha kikatili cha Rais Melchior Ndadaye. Hata walioitawala nchi mfano Petro Buyoya na Jean Baptiste Bagaza wanaombwa kueleza na kuonyesha ile Kamati ya Umoja na Maridhiano (CVR) yaliko mashimo walikozikwa watu wengi tangu uhuru wa nchi wakianzia kwa watoto wa Hayati Ludoviko Rwagasore, Waziri Mkuu Petro Ngendandumwe, Mfalme Ntare V Charles Ndizeye, nakadhalika kwani wanapajua ;
6. Chama CNDD-FDD kinajulisha kuwa yanayotokea yanaonyesha uhusika wa Rais wa Rwanda Paul Kagame hasa kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa baadhi ya wakimbizi na kuwachochea kurudi kufanya uhalifu na mauaji nchini Burundi ;
7. Chama CNDD-FDD kinahitimisha tangazo hili kwa kuomba kwa mara nyingine tena Mataifa kuitambua nchi ya Burundi. Nchi zilizosimamisha misaada ya miradi ya maendeleo wasitishe hatua hiyo ya vikwazo dhidi ya Burundi, kwani vigezo vya maamuzi yao vilitoka kwao kutokana na taarifa potovu na kwamba nchi ilijengewa hoja za visingizio na hadaa ili kuiangusha serikali. Hivyo budi warejeshe urafiki na ushirikiano kama ilivyokuwa awali, aidha warundi wanastahili kulipwa fidia kwa usumbufu waliosababishiwa. Ukweli umeanza kudhihirika! Kwa mara nyingine tena chama CNDD-FDD kinawapa pole familia zote waliopoteza wapendwa wao katika vurugu zilizosababishwa na maadui wa nchi na demokrasi.

Imetolewa Bujumbura, tarehe 02 Machi , 2016
na Mwenyekiti wa chama CNDD-FDD
Mheshimiwa Pascal Nyabenda

2 mars 2016

About Author

Evelyne


Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *