Tangazo

TANGAZO N° 002/2016 LA CHAMA CNDD-FDD LA TAREHE 02 FEBRUARI, 2016.

Mkutano wa 26 wa Marais wa Umoja wa Afrika ulionyesha kuwaelewa Warundi, nao wananchi watayafanyia kazi maazimio .

  1. Tangu mwezi Mei 2015, kumekuwepo na mfululizo wa mikutano ya Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wakuu wa Umoja wa Afrika hata mikutano ya Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu masuala ya Burundi. Nchi hii ilifuatiliwa sana ikabainika kwamba kulikuwa na maandalizi maovu dhidi yake ya baadhi ya mataifa ya Ulaya, Amerika na Rwanda. Katika vipindi vyote, pande mbili zilijitokeza wakati wa mikutano iwe tarehe 13 Mei, 2015 katika mkutano wa Wakuu wa Nchi uliofanyika Dar-es-salaam, katika Mkutano wa Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Dar-es-salaam tarehe 31 Mei, 2015 hata katika mkutano wa tarehe 13 Juni, 2015 kati ya Viongozi wa Umoja wa Afrika uliofanyika Johanesbourg Afrika Kusini na mikutano mingineyo. Ilikuwepo pia mikutano ya Kamati ya Usalama ya Umoja wa Mataifa (UN) na wakati wote walijitokeza waliotaka kukiuka haki za warundi na wengine wanaopenda warundi waheshimiwe kwa haki zao. Katika mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi uliofanyika Addis-Abeba kuanzia tarehe 30 – 31 Januari, 2016, wapo wajumbe waliounga mkono wazi wazi na kikamilifu nchi ya Burundi ili itoke katika migogoro ya kisiasa na usalama mdogo vinavyoisibu kwa kuheshimu uhuru na kujitawala kwa Taifa. Chama CNDD-FDD kinatumia fursa hii muhimu kuwashukuru kwa dhati Wakuu wa nchi, Jumuiya za kikanda ambazo Burundi ni mwanachama, mataifa pamoja na Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuzingatia Azimio No 2248 la 12 Novemba, 2015 lililodhihirisha kwamba hatimaye lilielewa wazi matatizo ya Burundi ingawa kulikuwa na uongo mwingi na propaganda vilivyokuwa vinaenezwa dhidi ya Burundi ili kudhalilisha wananchi kwa lengo la kuiweka nchi chini ya utawala wa kikoloni na majeshi ya kimataifa ;
  2. Kama methali isemavyo : Rafiki wa kweli huonekana wakati wa shida. Chama CNDD-FDD kinajua kwamba nchi hizo tofauti na wananchi wake nao kwao wana matatizo na majukumu mengi ya kufanya katika mataifa yao, lakini waliendelea kuunga mkono nchi ya Burundi kwa malengo ya kutaka itoke kishujaa katika wakati mgumu, hususan katika maamuzi ya hitimisho la Mkutano wa 26 wa Umoja wa Afrika. Maamuzi yaliyoafikiwa ni mazuri ya heshima, ya kutia moyo wananchi, nguvu na utashi wa kusonga mbele katika mazungumzo ya Warundi ;
  3. Pamoja na hayo chama CNDD-FDD hakikufurahishwa na baadhi ya nchi, asasi kadhaa pamoja na baadhi ya vyombo vya habari vya Ulaya ambavyo havikuchoka kuonyesha mienendo ya ukoloni kwa kupiga vita chama CNDD-FDD na serikali yake. Matendo ya aibu ya Samantha Power, Louis Michel na washirika wake na Paul Kagame yalidhihirika kwa kutaka kuisambaratisha demokrasi katika msingi wake nchini Burundi hivyo kuweka serikali ya Mpito ya kugawana madaraka ikiongozwa na Petero Buyoya. Huyo amefanya mapinduzi mara tatu, hadi sasa anataka kurejeshwa madarakani mara ya nne kwa kutumia makundi ya G7 na G10. Isingekuwa kusimama imara, kuipenda nchi na demokrasi vya wananchi wa Burundi na kupangua mitego iliyokuwa imewekwa na akina Petero Buyoya janga lingeifikia nchi. Chama CNDD-FDD kinashukuru wanachama wote, marafiki wa chama na wananchi kwa ujumla waliyoendelea kukiunga mkono chama na kuepuka kufarakana, wakadumu pamoja katika umoja na mshikamano ;
  4. Chama CNDD-FDD kinalaani na kukemea mawazo ya kikoloni ya rais Paul Kagame wa Rwanda ya kuandaa mpango wa kuishambulia Burundi ili itawaliwe kwa misingi ya kikabila kiujanja kama walivyofanya wakati wa RPF-Inkotanyi. Wapenzi wa demokrasi wa Burundi wanaikumbusha Rwanda kwamba isingekuwa usaidizi na kuungwa mkono kisiasa na kijeshi na MINUAR, kamwe RPF isingeshika madaraka nchini Rwanda ingawa pia alitumia siasa ya mauaji ya halaiki ili baadhi ya wanyarwanda wawe kafara iwezekane aitawale nchi. Mbinu hiyo ndiyo aliyotaka kutumia nchini Burundi, ambapo imedhihirika kuwa neno « Mauaji ya halaiki » lilipotumiwa yalikuwa maandalizi kwa warundi na mataifa kwa waliotarajia kufanya huku wakibebesha uovu huo kwa chama CNDD-FDD na serikali yake. Hayo yamewashinda ila wamebainika ;
  5. Inasikitisha kuona kwamba rais Paul Kagame pamoja na kuchangia uvunjifu wa amani nchini Burundi, hakuna aliyelaani au kukemea uovu huo, iwe kutoka Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa pamoja na Asasi za Kimataifa za Haki za Binadamu. Mashirika hayo yaliendelea kutaka kuirudisha katika ukoloni nchi ya Burundi kwa mapendekezo yao ya kupeleka vikosi vya majeshi ya kimataifa nchini Burundi. Wapenzi wa demokrasi waliona jinsi MINUAR ilivyoiweka madarakani RPF nchini Rwanda. Jeshi hilo la kimataifa nchini Burundi lisingekuwa na kazi nyingine bali kumrejesha madarakani Petro Buyoya ambaye anaonekana kuwa kinara wa makundi ya G7 na G10. Naye Kagame anataka kuleta Burundi yaliyofanyika nchini mwake. Alijaribu kuanzisha makundi ya wapiganaji kwa baraka za baadhi ya wanasiasa wa Ulaya tukianzia na Louis Michel na washirika wake katika fikra zake za kurejea madarakani kwa njia ya G7 na G10, hapa Buyoya akitumia njia ya mapinduzi kupitia serikali ya mpito. Hivyo neno « Mauaji ya halaiki na Ukabila » vinavyotumiwa ni visingizio na gia za wanasiasa uchwara wasio na sera kwa wananchi na wenye uchu wa madaraka bila kutoa jasho ;
  6. Waliokuwa wameandaa mauaji ya halaiki kama mtaji wa biashara waliishia kuaibika, wakaanza kusema habari ya mashimo walikozikwa watu wengi kama mradi mpya wa biashara. Kwa mara nyingi tena, Mashirika ya Kimataifa kama ya Haki za Binadamu kwa kutumia vyombo vya habari vya kimataifa na teknolojia ya mawasiliano ya kisasa vilidai kuwa kuna mashimo mapya ambapo pamezikwa watu wengi kwa pamoja. Yote hayo kwa lengo la kutokanusha au kujirudi kwa uongo wao wa mauaji ya halaiki uliowekwa wazi. Mauaji hayo ya halaiki hayakutokea na hali hiyo ingesababisha kuletwa vikosi vya Kimataifa nchini. Watu hao wanaopika uongo huo wanadai kuwa satelaiti ziliona picha za mashimo, hayo yote ni kutaka vile vikosi vya kimataifa vitumwe Burundi ili viunge mkono watu wao hivyo waingie madarakani kwa nguvu na kusababisha yale mauaji ya halaiki wanayoimba. Tarehe 17 Desemba, 2015 Petro Buyoya na washirika wake walidai kuwa yanafanyika mauaji ya halaiki nchini, naye Kagame alipongeza kuwa amepata « wanafunzi wazuri wa  mauaji ya halaiki». Mapya sasa katika kutafsiri mauaji ya halaiki ni – kutumia mashimo walikozikwa watu wengi !.Wanasahau historia ya nchi inayoonyesha kuwa kuna mashimo mengi sehemu mbalimbali walikozikwa watu wengi kwa pamoja hapa nchini. Kwa hiyo suala la mashimo hayo ni kazi ya Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu (CNIDH) na Kamati ya Ukweli na Maridhiano (CVR). Hakuna mwingine aliye na ruhusa ya kuingilia kamati hizo. Kwa nini maadui hao wanatumia neno mauaji kama njia ya kutaka kushika uongozi ? ;
  7. Kwa upande mwingine vyombo vya habari vya Ulaya vilitumiwa na wanasiasa wabaya kama Louis Michel walipomtumia Bernard Maingain na Televisheni France 3 kwa utapeli ili kupaza sauti na kelele kuwa mauaji ya halaiki yanafanyika. Mauaji hayo yalikuwa yametajwa na Louis Michel na Marguerite Barankitse katika mkutano wao wa Louvain-La Neuve tarehe 17 Desemba, 2015 ambapo kesho yake tarehe 18 Desemba 2015, wazo la MAPROBU liliibuka ghafla kutoka Umoja wa Afrika hususan kwa Nkosazana Dlamini-Zuma na Smail Chergui kwamba vitumwe vikosi vya askari 5000 vya kimataifa kwenda kuondoa na kusambaratisha mamlaka za uongozi uliochaguliwa na wananchi kidemokrasi. Hivi ndivyo Umoja wa Afrika unavyoiona demokrasi nchini Burundi. Umoja wa Afrika usiosema neno dhidi ya Rwanda kwa kuhusika na uvunjifu wa Amani nchini Burundi bali kuunga mkono nchi hiyo katika fikra za kikabila. Inatia aibu ;
  8. Chama CNDD-FDD kinawashukuru na kuwapongeza wote waliosimama imara kama viongozi mashujaa wa Afrika mfano RWAGASORE, NDADAYE, Kwame NKRUMAH, NYERERE, MANDELA, KADHAFFI na wengineo waliopinga mawazo ya kikoloni na kuhimiza uhuru na kijitawala kwa wananchi pamoja na mshikamano kama ilivyo katika wazo la kufanya kazi kwa pamoja (Panafricanisme) kama ilivyo wakati huu pia inavyohitajika;
  9. Tangazo hili haliwezi kuhitimishwa bila chama CNDD-FDD kuwashukuru wanachama wake wote ambao wanaendelea kushikamana na kukiunga mkono kwa moyo wote chama CNDD-FDD. Wananchi wanadumu katika umoja wao na kuipenda nchi yao. Chama CNDD-FDD kinawajulisha kwamba yaliyoafikiwa katika kilele cha mkutano wa 26 wa Umoja wa Afrika kuwa ni matokeo ya msimamo wenu. Chama CNDD-FDD kinavishukuru vikosi vya Ulinzi na Usalama waliopo na waliotutangulia kwa ushujaa na kujitoa kwao katika kutekeleza majukumu yao, ndivyo vilivyoleta majibu ya heshima kwa Taifa. Chama CNDD-FDD kinamalizia kwa kuwashukuru kwa moyo wa dhati Wakuu wa Nchi waliotambua mapema na kusaidia kuwaelewesha vizuri wenzao wa Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Burundi na mwafaka unaofaa kuwa ni katika mazungumzo ya warundi ili demokrasi izidi kuimarika nchini.

 

Imetolewa Bujumbura, tarehe 2 Februari, 2016

na Mwenyekiti wa chama CNDD-FDD

Mheshimiwa Pascal Nyabenda.

3 février 2016

About Author

Willy


Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *